Wadau wa maliasili na mazingira mkoani Iringa wamelilalamikia baraza la mazingira la taifa (NEMC) kwa kutozingatia kanuni, sheria na taratibu za utunzaji wa mazingira kwa kushindwa kuwadhibiti wananchi na wawekezaji wanaoendesha shughuli zao katika maeneo yasiyorafiki kwa utunzaji wa mazingira.
Malalamiko ya wadau yamekuja kufuatia mazungumzo ya wadau hao katika mkutano uliowakutanisha na uongozi wa mkoa huo wenye lengo la kujadili namna ya kukabilina na changamoto ya uharibifu wa mazingira hususani kuharibiwa kwa vyanzo mbalimbali vya maji pamoja na uchimbaji madini katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo.
Akizungumizia kuhusu kero za wadau hao mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela ameahidi kulifikisha suala hilo mahali husika ili kupunguza usumbufu wawekezaji na wananchi pamoja na kufanya tathmini ya athari za mazingira kabla ya kuanza shughuli za uzalishaji ama ujenzi.
Hata hivyo Kasesela ametoa muda wa miezi mitatu kwa wananchi na wawekezaji wanaokata miti kwa ajili ya shughuli mbalimbali kuhakikisha kabla ya kukata mti wanapata kibali kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya huku Afisa mazingira wa wilaya hiyo akisisitiza upandaji wa miti katika maeneo yanayokatwa miti ili kuendelea kuhifadhi mazingira.
Katika maeneo mengi nchini wananchi wamekuwa wakivamia mistu kwa kukata miti pamoja na kuendeleza shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji hali inayosababisha mabadiliko ya tabia nchi katika mikoa mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment