Wabunge wanaoendelea kujadili mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/2017, wameonesha kutoridhika na mapendekezo ya Serikali kuongeza kodi katika nguo za mitumba, katika huduma za utalii na bidhaa zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi.
Mbali na kupinga kodi hiyo, pia wawakilishi hao wa wananchi, wamesisitiza umuhimu wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), kuongezewa fedha.
Hata hivyo, wabunge hao wameonekana kutofautiana katika uamuzi wa Serikali kuwakata kodi; baadhi wakiunga mkono huku wakitaka makato hayo yafanyike hata katika kiinua mgongo cha marais, makamu wa rais, mawaziri wakuu, maspika na naibu maspika, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa.
Kwa upande wa mitumba, serikali katika bajeti yake, imependekeza kupandisha ushuru wa nguo na viatu vya mitumba kutoka dola za Marekani 0.2 mpaka dola za Marekani 0.4 kwa kilo, kwa nia ya kudhibiti nguo hizo lakini pia imetangaza kujiandaa kuzuia uingizaji wake.
Wakichangia juu ya hilo, Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM), alisema pamoja na kuwa hatua hiyo ni sehemu ya makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya Afrika Mashariki (EAC), Serikali inapaswa kuangalia suala hilo, kwa kuwa mitumba ni ajira ya vijana.
Alisema baadhi ya nchi hizo kwao ni rahisi kuzuia mitumba, kwa kuwa wameshajiandaa kuwa na viwanda vya nguo, wakati Tanzania bado haijafanya maandalizi yao.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alipinga kuwekwa kwa kodi hiyo na kuhadharisha kuwa, kodi hiyo itaua biashara ndogo, ikiwemo masoko ya mitumba na kuongeza vibaka barabarani.
Kwa upande wa kodi ya utalii, katika mapendekezo ya Bajeti ya Serikali, Serikali ilikusudia kukata asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika huduma za utalii, lakini Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM), aliipinga akisema Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, alitaja kodi hiyo na kusema hata Kenya, Afrika Kusini na Rwanda, wanayo.
Mapunda alisema kwa kuwa Kenya wameshaondoa VAT katika utalii, ni vyema sasa na Tanzania ambayo sekta hiyo ni ya pili katika ukuzaji wa uchumi, iondoe kodi hiyo ili kuilinda dhidi ya washindani.
Naye Bashe katika tozo hiyo ya utalii, alionya kuwa Tanzania pamoja na kuwa na vivutio vingi, kunaweza kuwa eneo ghali kwa mtalii kutembelea kwa kuwa nchi washindani katika biashara za utalii, wameweka tozo hiyo pembeni.
Wakati huo huo katika hatua iliyoonekana kuwaunganisha wabunge wote, ni ya kumuongezea fedha CAG, ambaye imeelezwa aliomba zaidi ya Sh bilioni 60 lakini akaambulia takribani Sh bilioni 30 tu.
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly (CCM) alimtaka Waziri wa Fedha na Mipango, kueleza kama CAG ni adui wa Serikali au ni shetani?
Kwa mujibu wa mbunge huyo, ambaye pia ndiye Makamu Mwenyekiti wa Kamati wa Bunge ya Hesabu za Serikali, alisema fedha zilizotengwa kwa ajili ya CAG, ni za mishahara na uendeshaji wa ofisi yake.
Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM), yeye alihoji kama fedha zilizotengwa kwa CAG, zinatosheleza kumsaidia akague wizara zote, mashirika na idara zote za Serikali na miradi ya maendeleo, ambayo bajeti hiyo imekusudia itengewe asilimia 40 ya fedha zote.
Hasunga alikwenda mbali zaidi na kusema kama fedha za CAG hazitatosha na kumlazimu kwenda kuomba serikalini, uhuru wake ambao haupaswi kuingiliwa, utakuwa mashakani na wakati mwingine, anaweza kulazimika kukubali kuathiri uhuru huo ili apewe fedha.
Mbunge huyo alimtaka Waziri wa Fedha na Mipango, aeleze kama sababu ya kumnyima CAG fedha, ni matokeo ya kubainika akitumia vibaya fedha alizowahi kutengewa huko nyuma.
Mbunge wa Nzega Mjini, Bashe alihoji iweje Hazina na Mamlaka ya Mapato (TRA), wakimbizane kukusanya fedha, kisha CAG akatwe miguu.
Mbunge huyo wa Nzega, alishauri fedha zilizokuwa zipelekwe katika ununuzi wa mabehewa na vichwa vya treni Sh bilioni 161, zipunguzwe na kupelekwa kwa CAG, kisha TRL iruhusiwe kwenda kukopa katika benki.
Kodi ya petroli
Wakati Serikali kwa makusudi ilikwepa kuongeza kodi mpya katika mafuta ya petroli na dizeli kwa nia ya kuepuka mchango wake katika mfumuko wa bei, wabunge wametaka kuongezwe tozo mpya ya Sh 50 kwa kila lita ya petroli na dizeli kwa manufaa ya wananchi.
Mbunge wa Makete, Dk Norman Sigala (Makete), aliunga mkono maoni ya Kamati ya Bajeti ya kutaka fedha hiyo katika mafuta, ikatwe ipelekwe kwenye miradi ya maji, huku akihoji kigugumizi kiko wapi wakati tozo hiyo inarudi kwa wananchi?
Kiinua mgongo
Kuhusu kiinua mgongo, wabunge wengi wameonesha kuguswa huku wengine wakiweka wazi kuwa Serikali imeshika pabaya, panapouma na wengine wakisema huenda sababu ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mpango kwa madai kuwa hajui uchungu wa jimbo.
Mbunge Zungu wa Ilala, alisema katika miaka mitano, wabunge hulipa kodi inayofikia Sh milioni 50 na kuiomba Serikali kufikiria upya suala hilo la kuwakata kodi ya kiinua mgongo.
Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda (CCM), alisema kodi hiyo ya kiinua mgongo inakatwa hata kwa watumishi na kushangaa kwa nini watumishi na wabunge ambao wamekuwa wakilipa kodi katika mishahara, wakatwe tena kodi katika kiinua mgongo.
Mbunge wa Nzega Mjini, Bashe alisema ili kuwe na usawa katika sheria, ni vyema kodi hiyo ya kiinua mgongo, ikatwe kwa viongozi wote wa kisiasa, kuanzia marais makamu wa rais, mawaziri wakuu, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, maspika na naibu maspika.
Alisema anaona kuwa wabunge katika hilo wanachonganishwa na wananchi, hivyo ni bora wabunge wakubali kulipa kodi hiyo, lakini iwahusu viongozi wote wa kisiasa.
Mbunge Hasunga, alieleza kushangazwa kusikia kodi hiyo imeletwa katika bajeti ya 2016/17 wakati itapaswa kukatwa mwaka wa mwisho wa utumishi wao na kuhoji, kwa nini imeletwa mwaka huu wakati haiwezi kutozwa mwaka huu.
Mbunge wa Viti Maalumu, Jacqueline Ngonyani (CCM), alikwenda mbali na kusema Serikali imegusa pabaya, panauma na hasa kwake ambaye hana jimbo, ila anahudumia mkoa mzima kwa kuwa sehemu ya mapato yake, anayatumia kuhudumia wananchi na kudai kuwa mpaka jana saa tano asubuhi, alikuwa kapigiwa zaidi ya simu 50 na wananchi wakiomba msaada.
Mbali na huyo, Mbunge Hilaly wa Sumbawanga Mjini, alisema Msemaji wa Kambi ya Upinzani, David Silinde, alisema Chadema inaunga mkono kukatwa kodi ya kiinua mgongo na kutaka mbunge huyo wa Momba, aandike barua kwa Spika kuridhia kodi hiyo, ili yeye Hillaly awe wa pili kuandika.
Alitoa kauli kwa ufupi tu kuwa kodi hiyo ifutwe na kuongeza kuwa huenda imewekwa kwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mpango hajui uchungu wa jimbo, kwa kuwa yeye ni Mbunge wa kuteuliwa na Rais.
No comments:
Post a Comment