Tafrani limeibukia Klabu ya Yanga kuhusu Uchaguzi Mkuu wao baada ya Leo Uongozi wao kujitokeza na kutangaza mchakato wa Uchaguzi huo huku TFF nao wakitoa Taarifa ya mwendelezo wao wa kuusimamia Uchaguzi huo bila Uongozi wa Yanga kuhusishwa.
Hii Leo, Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, amesimama na kueleza maagizo aliyopewa na Kamati ya Uchaguzi ya Klabu na Bodi ya Wadhamini kutangaza kuhusu Uchaguzi wao huku akibainisha hawana imani na TFF na hawako tayari kusimamiwa na TFF kwenye Uchaguzi wao wenyewe.
Yanga imetamka Uchaguzi upo Juni 11 na si Juni 16 kama usimamizi wa TFF unavyoamrisha.
Pia Katibu Mkuu huyo ameelezea kuhusu mchakato wao wa Uchaguzi ambapo Fomu kwa Wagombea zitatolewa Juni 2 na 3, Juni 4 ikiwa ni Kikao cha Mchujo wa Wagombea.
Zoezi hilo, Yanga imenena, litasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga na Sekretarieti yake.
Juni 5 ni Siku ya kupokea pingamizi zozote huku Juni 6 ikiwa ni Siku ya kuzipitia na kufanyika kwa usaili na baada ya hapo Majina ya Wagombea kupelekwa TFF kuhakikiwa na kutolewa maamuzi ya Maadili.
Katibu Mkuu Baraka ameeleza: “Hiyo ni pamoja na kukata rufaa kwa maamuzi yaliotolewa, kusikilizwa rufaa na kutoa maamuzi ya rufaa na kisha kutangaza majina ya wagombea, zoezi ambalo sasa watafanya TFF na huo ndiyo utaratibu wa siku zote,"
Yanga imeendelea kueleza Juni 7 mpaka 10 ni Kampeni kwa Wagombea kujitangaza kwenye Matawi yao.
Juni 11, kwa mujibu wa Yanga, ndio Uchaguzi wakati TFF wakibaki waangalizi tu.
TAARIFA YA TFF:
UCHAGUZI YANGA UNASIMAMIWA NA TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linapenda kuwafahgamisha wanachama wa Young Africans na familia ya mpira kwa ujumla kuwa mchakato wa uchaguzi wa Klabu ya Young Africans unaendelea vizuri na unasimaiwa na Kamati ya Uchaguzi ya shirikisho kwa mujibu wa utaratibu ulioutoa awali.
Fomu za uchaguzi zinaendelea kuchukuliwa katika ofisi za Makao Makuu ya TFF-Karume. Vilevile fomu zinaweza kupatikana kwenye tovuti ya TFF amayo ni www.tff.or.tz.
TFF inafuatilia kwa karibu mwenendo mzima wa mchakato na taarifa zote zitatolewa na TFF kupitia wasemaji wake na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ambaye ni Wakili Msomi, Alloyce Komba.
Tayari Kamati ya Uchaguzi ya TFF, iliyopewa jukumu la kusimamia uchaguzi wa Klabu ya Young Africans imeridhishwa na mwenendo wa wanachama kwa namna wanavyochukua na kurejesha fomu.
Na kutokana na mipango yake, imesogeza mbele mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu mpaka Jumatatu Juni 6, 2016 saa 10:00 jioni.
Hadi sasa wanachama tisa (9) wamechukua na kurejesha fomu. Wanachama hao ni Aaron Nyanda na Titus Osoro wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti kwa mujibu wa katiba ya mwaka 2010 inayotambulika serikalini hadi sasa.
Wengine ni Paschal Laizer, Edgar Chibula, Mohammed Mattaka, Mchafu Ahmed Chakoma, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ Omari Said kutoka Zanzibar. Uchaguzi wa Yanga unatarajiwa kufanyika Juni 25, 2016.
Fomu zinapatikana katika ofisi za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam. Vilevile utaratibu unafanyika ili fomu ziweze kupatikana katika tovuti ya shirikisho www.tff.or.tz
Fomu zinapatikana kwa gharama ya Sh 200,000 kwa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti na Sh 100,000 kwa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji.
No comments:
Post a Comment