Latest News

Thursday, July 28, 2016

Safari ya Dodoma kwa viongozi wa Tanzania inapamba moto!

Siku chache baada ya Rais John Magufuli kutangaza azma yake ya kuhamishia ofisi yake mkoani Dodoma, mawaziri wake sasa wako mbioni kumfuata kutekeleza agizo lake.
Dhamira ya Rais Magufuli iliungwa mkono na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyesema atahamia Dodoma ifikapo Septemba.
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba, yeye alisema atahamia Dodoma wiki ijayo.
Wakizungumza kwa simu jana, baadhi ya mawaziri walisema suala hilo halina mjadala bali ni utekelezaji tu.
Naibu Waziri (Ofisi ya Waziri Mkuu), Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Dk Abdallah Possi alisema wamekuwa na vikao katika wizara hiyo vya kujipanga kuhamia Dodoma.
“Tangu juzi Ofisi ya Waziri Mkuu tulikuwa na vikao na hata leo (jana) tumekuwa na vikao na wafanyakazi, yote ni kujadili namna ya kuhamia Dodoma,” alisema Dk Possi.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge alisema suala hilo ni agizo lisilo na mjadala.
 Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba alisema bado wanajipanga kutekeleza agizo hilo.
“Hayo ni maelekezo siyo suala la kuunga mkono, sisi lazima tuyatekeleze. Bado tunajipanga, tukishamaliza tutatoa taarifa rasmi.” alisema Makamba.

No comments:

Post a Comment