Latest News

Thursday, August 11, 2016

Taarifa Toka IKULU Kuhusu Maagizo ya Rais Magufuli Aliyoyatoa Jana Jijini Mwanza


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vya dola kuchunguza na kuchukua hatua za kurejesha mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha  Nyanza ambazo zilinunuliwa na kutwaliwa na watu binafsi kwa njia za ujanja ujanja.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo tarehe 11 Agosti, 2016 alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Mwanza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.

Dkt. Magufuli alisema Serikali yake haipo tayari kuwafumbia macho watu wachache waliovifilisi vyama vya ushirika vya wakulima kwa kujimilikisha mali za ushirika yakiwemo majengo, viwanda na mashamba na ametaka mali hizo zirudishwe mikononi mwa wananchi.

"Hata kama walichukua miaka 20 iliyopita, vyombo vya dola vichukue hatua na mali hizo zirudishwe kwa umma" Alisema Rais Magufuli.

Katika Mkutano huo Rais Magufuli pia alisema Serikali itafanya oparesheni kubwa ya kuteketeza Makokoro katika ziwa Victoria ikiwa ni juhudi za kukabiliana na tatizo la uvuvi haramu uliosababisha kupungua kwa samaki na kuathiri shughuli za uvuvi na usindikaji wa minofu ya samaki katika viwanda.

Alibainisha kuwa lengo la kuchukua hatua hiyo ni kuwezesha samaki wengi kuzaliana ili lengo la Serikali la kujenga viwanda vya kusindika mazao ikiwemo viwanda vya kusindika minofu ya samaki lifanikiwe.

Kabla ya kuhutubia mkutano huo Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la waenda kwa miguu la Furahisha linalokatiza barabara ya Uwanja wa Ndege kwenda katikati ya Jiji la Mwanza.

Daraja hilo litakuwa na urefu wa meta 46, upana wa meta 3.6 na kimo cha meta 5.5 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika Mwezi Desemba Mwaka huu kwa gharama ya Shilingi Bilioni 6.455

Akizungumzia ujenzi huo Rais Magufuli alimtaka Mkandarasi anayejenga Daraja la Furahisha kukamilisha kazi hiyo Mwezi Desemba Mwaka huu kwa mujibu wa mkataba, na pia ameagiza Mkandarasi aliyekuwa akifanya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kuendelea na kazi hiyo ndani ya wiki moja kwa kuwa Serikali imejipanga kumlipa fedha za kazi hiyo.

Pia Dkt. Magufuli ameahidi kuongeza fedha katika ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Katikati ya Jiji la Mwanza hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza ili barabara hiyo ifike hadi uwanjani badala ya kuishia eneo la Pasiansi.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Mwanza

11 Agosti, 2016

No comments:

Post a Comment