Ikiwa bado kuna mkanganyiko wa mambo ndani ya chama cha CUF, Umoja wa Vijana wa CUF (JuviCUF) umewataka vijana wa chama hicho kutotoa ushirikiano kwenye ziara ya mwenyekiti aliyevuliwa uongozi na Baraza Kuu, Profesa Ibrahim Lipumba na baadhi ya wabunge inayotarajiwa kuanza wiki hii mikoa ya Lindi, Mtwara na Tanga.
Wito huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Juvi-CUF, Hamidu Bobali alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa ziara hiyo ina lengo la kukipasua chama hiko rasmi.
“Tunajua ziara hiyo inataka kuongeza mpasuko ndani ya chama na mpasuko huo utawapa mwanya maadui zetu ‘kutupiku’ kisiasa,” alisema Bobali.
Bobali, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mchinga kwa tiketi ya chama hicho, alisema pamoja na harakati za Lipumba tayari wabunge wa mikoa hiyo wapo katika kikao kuandaa mikakati ya kuimarisha chama.
Kadhalika Bobali alifafanua kuwa kama Jumuiya wanalaani kitendo kilichofanywa na kikundi cha vijana kilichojiita cha Mkoa wa Dar es Salaam cha kutoa kashfa kwa viongozi wa Ukawa akiwamo Freeman Mbowe na Julius Mtatiro.
Juvi-CUF iliwatoa hofu wananchi wa Zanzibar kuhusu hali ya kisiasa iliyopo visiwani humo, kutokana na hatua mbalimbali za kisheria zinazofuatwa ili kuhakikisha haki inapatikana kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Kuhusu sakata la akaunti ya chama inayoingizwa fedha za ruzuku na za wabunge, alisema hakuna fedha za wabunge zitakazoingia katika akaunti hiyo kutokana na mikataba inayosainiwa inahusu Mbunge na Ofisi ya Bunge na siyo chama.
“Tumechukua hatua kuwaeleza benki kuhusu akaunti kufunguliwa, suala hili linafanywa na bodi ya wadhamini inayoongozwa na Khatau hivyo siyo suala rahisi yeye (Lipumba) akazipata,” alisema Khatau.
No comments:
Post a Comment