Latest News

Saturday, October 8, 2016

Taarifa za kukodishwa kwa Yanga zina ufafanuzi wake hapa!

Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imesema kuwa mkataba wa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kukodishwa klabu hiyo ni batili. Tamko hilo limetolewa jana oktoba 7 na Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja baada ya juzi kusambaa kwa taarifa ya mkataba wa Yanga katika mitandao ya kijamii.
Suala la Yanga kukodishwa timu lilianza mchakato tangu Manji aitishe mkutano mkuu wa dharura miezi miwili iliyopita, akiomba ridhaa ya wanachama wa klabu hiyo kumkodisha timu na nembo kwa miaka 10, ombi ambalo lilipitishwa na kurudishwa katika bodi ya wadhamini kwa ajili ya kufanyiwa kazi na juzi kupitishwa kwa makubaliano hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kiganja alisema wanaunga mkono suala la mabadiliko, lakini lazima yafuate sheria na taratibu zilizowekwa ili kukamilisha mabadiliko yoyote.
“Mimi sipingi klabu zetu kufanya mabadiliko isipokuwa najaribu kukumbusha zifuate utaratibu wa kisheria, kwa sababu unapobadilisha jina au kufanya marekebisho yoyote ni lazima vikasajiliwe na kutambulika,”alisema.
Kiganja alisema hata Bodi ya Yanga iliyohusika kuruhusu timu hiyo kukodishwa haitambuliki kwa Msajili, kwa vile wajumbe wake wengi ni wale waliochaguliwa kwa mpito. Alisema bodi ya wadhamini iliyoundwa Julai 5, 1973 ni wawili tu wanaotambulika waliopo hadi sasa ambao ni Jabir Katundu na Juma Mwambelo.
Lakini, Mwembelo amekuwa ahusishwi tena katika mambo yanayoendelea ya timu hiyo. Bodi ya mpito, ambayo Kiganja alisema hawakusajiliwa wala kupitishwa kwenye mkutano mkuu kutokana na taratibu ni George Mkuchika, Fatuma Karume, Francis Kifukwe, Amri Ramadhan, Juma Kambi na Abeid Mohamed.
Katibu huyo alifafanua taratibu zinazotakiwa kufuatwa ili timu ikodishwe kuwa ni kutumia vikao, ambapo cha kwanza ikiwa ni Kamati ya Utendaji ya Klabu itakayochambua hoja na kukubaliana au kutokukubaliana kisha kupeleka katika kikao cha ngazi za juu.
Pia, alisema baadaye hoja inapelekwa kwenye mkutano mkuu wa wanachama wote uwe wa dharura au kawaida ili kujadiliana hoja husika, kisha baada ya kukubaliana au kutokukubaliana inapelekwa kwa Baraza la wadhamini lenye uwezo wa kuingia kwenye maamuzi makubwa, na mwisho inapelekwa kwa msajili.
“Kwa mujibu wa sheria ya BMT ya mwaka 1967 kifungu namba 11 (1) kinaeleza chama chochote kinachofanya mabadiliko ya jina, anuani, madhumuni au kifungu chochote cha Katiba yake kitatakiwa kipate idhini ya msajili,”alisema.
Alisema kifungu namba 11 (3) msajili anaweza kuyakataa maombi ya kubadili kifungu chochote cha katiba kama ataona kuwa mabadiliko yanaweza kuhatarisha usalama na kuvuruga amani, au kama kuna malengo ya kuwanufaisha wachache au kama hayazingatii sera za michezo na sheria za BMT.
Alisema baada ya hatua hizo kukamilika, inabidi kufanya marekebisho ya Katiba ambayo yatapitia kwenye taratibu za klabu, na ndipo klabu husika itakuwa imepata baraka za serikali.
Katibu huyo aliweka wazi kuwa amezungumza hayo kwa kuwa yeye ni kiongozi na mlezi wa vyama vya michezo nchini na kwamba, maelezo yake hayalengi kuwakatisha tamaa wale walionesha nia ya kuwekeza kwenye michezo bali kuwambushana mambo ya msingi kwa manufaa.

No comments:

Post a Comment