Watu watatu wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Tipa lenye namba za usajili T892 BRH walilokuwa wakisafiri nalo wakitokea kijiji cha Kisomachi kuelekea uchira, likiwa limebeba mawe kuacha njia na kugonga nyumba kisha kupinduka katika kijiji cha Uchira wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Baadhi ya mashuhuda wamesema gari hilo lilikuwa kwenye mwendokasi kwenye barabara itokayo shule ya sekondari uchira majira ya saa tisa alasiri, kisha likavuka kwenye barabara kuu itokayo Moshi na kuelekea Dar Es Salaam na kugonga nyumba ya Samwel Koka na kujeruhi watoto wawili ndani ya nyumba hiyo.
Mwanamazingira wa shule ya sekondari uchira Hadji Msofe, amesema gari hilo lilikuwa likipakia mawe kwenye eneo la shule bila idhini ya shule, na kwamba alitoa taarifa kwa mwalimu mkuu na walipojaribu kufuatilia, walikutana na gari hilo na dereva alikataa kusimama, na kuwapita kwa kasi.
Kaimu kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro Koka Moita amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo huku akiwataja waliofariki dunia kuwa ni dereva wa gari Francis Ngowi, Abiria Anderson John na abiria mmoja ambaye jina lake halijafahamika.
Majeruhi ni Daniel August ambaye ni abiria, Jackline Eliam na Irene Samwel ambao ni watoto wa mwenye nyumba.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya KCMC, na miili ya majeruhi inaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

No comments:
Post a Comment