Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) limeiondoa Klabu ya ES Setif ya Algeria katika hatua ya makundi ya michuano Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya mashabiki wake kufanya vurugu kwenye mchezo dhidi ya Mamelodi Sundown.
Timu yao ikiwa nyuma kwa mabao 2-0, Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa 8 Mai 1945 jijini Setif, Algeria, mashabiki wa ES Setif walivamia uwanjani dakika ya 90 na kufanya vurugu.
Mwamuzi Mahamadou Keita wa Mali alilazimika kusimamisha mchezo huo kwa muda na baada ya fujo kuisha akamaliza mechi.
Mabao ya Mamelodi yalifungwa na Tiyani Mabunda na Billiat Khama katika dakika za 33 na 63 na kuipa ushindi wa kihistoria timu yao ambayo ni maarufu kwa jina la Masandawana.
Taarifa iliyotolewa na Caf, jana Ijumaa ilisema: “Kutokana na vurugu zilizotokea katika mechi namba 98 ya Ligi ya Mabingwa 2016 kati ya ES Setif na Mamelodi Sundowns, ES Setif imeondolewa katika michuano hiyo kutokana na mashabiki wake kuhusika na vurugu hizo.
“Ripoti ya mwamuzi imeweka wazi kwamba, vitu vingi vilirushwa uwanjani ikiwemo silaha za moto, mawe, chupa na baruti na kusababisha majeraha kwa maofisa wa mechi hiyo.”
Kamati ya Mashindano ya Caf imetumia kanuni ya saba kifungu cha tatu cha michuano hiyo, kuitoa ES Setif katika Ligi ya Mabingwa ikianza kwa kuipokonya ushindi hata kama ingeshinda.
Kanuni hiyo inasema hivi: “Ikitokea mwamuzi akasimamisha mchezo na hatimaye kuuvunja kutokana na mashabiki kuvamia uwanja, timu mwenyeji itapokonywa ushindi na kuondolewa katika michuano.”
Kundi B la michuano hiyo sasa limebaki na timu tatu za Mamelodi, Enyimba ya Nigeria na Zamalek ya Misri. Jumatano ijayo, Mamelodi itacheza na Enyimba kwenye Uwanja wa Lucas Masterpieces Moripe jijini Pretoria, Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment