Latest News

Wednesday, June 1, 2016

Muhongo awataka wawekezaji kuchangamkia Nishati zilizogunduliwa


Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa   ili  Tanzania  iweze kuwa nchi ya  viwanda, nishati ya uhakika inahitajika  na kutaka makampuni kuwekeza katika uzalishaji wa umeme unaotokana na gesi.

Profesa Muhongo ameyasema hayo jijini  Dar es  Salaam   katika  nyakati  tofauti alipokutana na  watendaji wa kampuni zinazojishughulisha na  Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi  pamoja na wataalamu kutoka  Wizara ya Nishati na Madini na  Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) lengo likiwa ni  kupokea taarifa ya maendeleo ya miradi mbalimbali  ya makampuni hayo ambayo yanafanya kazi kwa kushirikiana na  Shirika la TPDC, British  Gas (BG),  Ophir,  ExxonMobil na Statoil.

Profesa Muhongo amesema kuwa hakuna nchi yoyote  duniani iliyopiga hatua kimaendeleo bila kuwa na nishati ya uhakika ya  umeme na kuwataka  wawekezaji kuchangamkia  fursa kupitia  gesi nyingi iliyogunduliwa.

Ametaja maeneo yanayohitaji uwekezaji   katika kuzalisha  umeme kwa kutumia gesi  kuwa ni pamoja na Mtwara,  Lindi, Somanga Fungu, na Mkuranga na kuongeza kuwa   viwanda  37 vya umeme wa gesi pamoja na vya sementi  vinahitaji  gesi na kusisitiza kuwa  iwapo sekta ya  gesi itatumiwa ipasavyo inaweza kuchangia nchi  kupiga hatua na kuingia katika  kundi la nchi zenye kipato cha  kati ifikapo mwaka 2025 kama  Dira ya Maendeleo  ya Taifa inavyosema.

Akizungumzia   mikakati ya serikali katika kuzalisha  wataalam  katika masuala ya mafuta na gesi Profesa Muhongo amesema kuwa serikali imekuwa ikitoa ufadhili kwa wanafunzi katika ngazi  za shahada za uzamili na uzamivu katika  vyuo  vilivyopo nje ya nchi  vyenye uzoefu katika  fani hiyo, pamoja na uanzishwaji wa programu hizo katika   Chuo Kikuu cha  Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha  Dodoma (UDOM) na  Chuo  cha Madini.

Naye   Mkurugenzi Mtendaji kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) Dk.  James Mataragio amesema kuwa  shirika  hilo  limekuwa likishirikiana na  kampuni hizo katika  hatua zote muhimu hususan katika kiwanda cha  kuchakata  gesi asilia  kimiminika (Liquefied Natural Gas) na  kuongeza kuwa mpaka sasa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda limeshapatikana.


Naye Meneja Mkazi wa Kampuni  ya  Statoil Tanzania, Øystein Michelsen, amesema kuwa kampuni yake  ipo  tayari kushirikiana na Serikali  kuhakikisha kuwa miradi yake inakamilika kwa wakati ambapo kampuni hiyo   imekuwa ikishirikiana na  Serikali kwa kutoa ufadhili wa masomo  katika masuala ya  gesi na mafuta nje ya nchi kwa wanafunzi wanaofanya  vizuri.

Ameongeza kuwa kampuni ya  Statoil imekuwa ikitoa elimu ya  ujasiriliamali kwa wakazi wa mkoa wa Mtwara  ili waweze kushiriki  katika uchumi wa gesi kupitia  utoaji wa  huduma  zake kwa Kampuni hiyo.

No comments:

Post a Comment