Mwili wa Francis Kanyasu maarufu Ngosha (86) anayedaiwa kuwa mbunifu wa nembo ya Taifa umeagwa leo (Jumamosi) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Ngosha alifikishwa hospitalini hapo Mei 25 akitokea Hospitali ya Rufaa ya Amana na alifariki dunia Mei 29 saa 2:30 usiku akipatiwa matibabu.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mungereza aliyemwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe katika kuaga mwili wa Ngosha amewataka wasanii kujiunga katika vyama vyao ili kujiweka katika mazingira rafiki ya utekelezaji wa majukumu yao, ikiwamo kusaidiana katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Mungereza amekaririwa na Idara ya Habari (Maelezo) akisema utaratibu wa kuwapo vyama vya wasanii ni wa muda mrefu tangu miaka ya sitini na wasanii wamekuwa wakijiunga kwa lengo la kuwa na sauti ya pamoja.
“Waziri anasema wazee wa namna hii na wasanii kwa jumla ni vizuri tukafuata utaratibu kwa mujibu wa sheria, hii itasaidia wasanii kutambulika, kujitangaza na kufahamiana,” amesema.
Daktari wa Magonjwa ya Dharura wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Juma Mfinanga amesema Ngosha amefariki dunia kutokana na maradhi ya Kifua Kikuu aliyougua kwa muda mrefu bila ya kupatiwa matibabu.
Dk Mfinanga ametoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kuwahi kufika katika vituo vya tiba wanapohisi kuwa na matatizo ya kiafya kwa kuwa kufanya hivyo kutawaweka katika mazingira mazuri ya kuepuka vifo visivyotarajiwa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Malapa, Buguruni alikokuwa akiishi Ngosha ameipongeza Serikali kwa jitihada za kuhakikisha inawapata ndugu zake, hivyo kusafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani kwao Kijiji cha Igokero wilayani Misungwi mkoani Mwanza.
No comments:
Post a Comment