Diwani wa Chadema, kata ya Bangata wilayani Arumeru (Arusha)
Emmanuel Mollel amejiuzulu nafasi yake ikiwa ni siku chache baada ya kutuhumiwa
na uongozi wa chama hicho kwa utovu wa nidhamu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru,
Christopher Kazeri amethibitisha taarifa za kujiuzulu kwa diwani huyo na kusema
kwamba ofisi yake imepokea taarifa za kujiuzulu kwake.
Mollel alipotafutwa kwa njia ya simu leo,
Juni Mosi, 2017, alikiri kuandika barua ya kujiuzulu huku akisema kwamba
amefanya uamuzi huo kwa utashi wake binafsi lakini akakanusha kupewa barua
yoyote ya onyo na uongozi wa chama hicho.
Katibu wa Chadema mkoani Arusha,Aman
Gorugwa amethibitisha taarifa za kujiuzulu kwa kiongozi huyo na kusema kuanzia
leo Mollel sio mwanachama wa Chadema tena.
Gorugwa amesema kwamba uongozi wa chama
chao ulimwandikia barua hivi karibuni ya kumtaka ajieleze sababu za
kutowajibishwa kutokana na tuhuma zinazomkabili.
Ametaja tuhuma hizo kuwa ni pamoja
na utovu wa nidhamu,mwenendo usiofaa ,kwenda kinyume na maagizo ya
chama na usaliti.
Amesema hata kabla ya kujibu tuhuma hizo
walipokea barua ya kujiuzulu kwake.
Katibu huyo amesema kwamba jina la Mollel lilikuwa kwenye orodha ya kitabu
cheusi (black book) na alikuwa kwenye hatua za mwisho za kutimuliwa.
Source: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment